Ufunuo wa Yohana Mtakatifu.
Kitabu cha Ufunuo.
William Branham.Kusoma kamili ya akaunti katika...
Ufunuo wa Yesu Kristo.Ufunuo 1:1-3,
“Ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na Mungu awaonyeshe watumwa wake mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi; naye akatuma kwa mkono wa malaika akamwonyesha mtumwa wake Yohana;
Aliyelishuhudia Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu Kristo, yaani, mambo yote aliyoyaona.
Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu.”Mwandishi (si mwanzilishi) wa kitabu hiki ni mtauwa Yohana Mt.. Wanahistoria wanakubaliana ya kwamba yeye aliishi sehemu ya mwisho ya maisha yake huko Efeso, ingawa katika wakati wa kuandika kitabu hiki yeye alikuwa katika Kisiwa cha Patmo. Si hadithi ya maisha ya Yohana, bali ni Ufunuo wa Yesu Kristo katika nyakati za kanisa zijazo. Katika aya ya tatu unaitwa unabii na ndivyo ilivyo hasa.
Kitabu hiki kwa kawaida huitwa Ufunuo wa Yohana Mtakatifu, lakini hilo si sahihi. Ni Ufunuo wa Yesu Kristo aliopewa Yohana kwa ajili ya Wakristo wa nyakati zote. Ndicho kitabu pekee katika Biblia nzima ambacho kimeandikwa na Yesu Mwenyewe, kwa kumtokea mwandishi Yeye Mwenyewe.
Ndicho kitabu cha mwisho cha Biblia, hata hivyo kinasimulia mwanzo na mwisho wa nyakati za Injili.
Sasa neno la Kiyunani la ufunuo ni “apocalypse” ambalo maana yake ni “kufunuliwa”. Kufunuliwa huku kunaelezewa kikamilifu katika mfano wa mchonga sanamu akifunua kazi yake ya sanamu, akiianika kwa mtazamaji. Ni kufunua, kuonesha kile kilichokuwa kimefichwa hapo awali. Sasa kule kufunua si tu ufunuo wa Utu wa Kristo, bali ni UFUNUO WA KAZI ZAKE ZIJAZO KATIKA ZILE NYAKATI SABA ZIJAZO. Umuhimu wa ufunuo wa Roho kwa mwaminio wa kweli hauwezi kamwe kutiliwa mkazo sana. Ufunuo unamaanisha mengi zaidi kwako labda kuliko unavyotambua. Sasa sizungumzi juu ya Kitabu hiki cha Ufunuo na wewe. Ninazungumza juu ya mafunuo YOTE. Ni muhimu sana kwa kanisa. Je! unakumbuka katika Mathayo 16 ambapo Yesu aliwauliza wanafunzi swali hili,
“Watu husema mimi Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Nao wakasema, Wengine husema ya kwamba Wewe u Yohana Mbatizaji; wengine Eliya; na wengine, Yeremia, ama mmoja wa manabii. Akawaambia, Lakini ninyi je, mwasema mimi kuwa ni nani? Ndipo Simoni Petro akajibu akamwambia, “Wewe Ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Naye Yesu akajibu akamwambia, “Heri wewe, Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba Yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, ya kwamba wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa Langu; wala malango ya kuzimu hayatalishinda.”
Wakatoliki wa Kirumi wanasema ya kwamba kanisa limejengwa juu ya Petro. Sasa hilo kwa kweli ni la kimwili. Mungu angewezaje kulijenga kanisa juu ya mtu asiye na msimamo hata akamkana Bwana Yesu na kulaani wakati akifanya jambo hilo? Mungu hawezi kulijenga kanisa Lake juu ya mtu yeyote aliyezaliwa katika dhambi. Wala haikuwa ni mwamba fulani uliokuwa umelala pale kana kwamba Mungu alikuwa ameitakasa ardhi ya mahali pale. Na si kama Waprotestanti wanavyosema, kwamba kanisa limejengwa juu ya Yesu. Ilikuwa ni UFUNUO. Lisome jinsi lilivyoandikwa: “Mwili na damu HAVIKUKUFUNULIA hili, BALI BABA YANGU NDIYE ALIYEKUFUNULIA, na JUU YA MWAMBA HUU (UFUNUO) NITALIJENGA KANISA LANGU:” Kanisa limejengwa juu ya Ufunuo, juu ya “Bwana Asema Hivi”.
Habili alijuaje la kufanya ili kumtolea Mungu dhabihu ifaayo? Kwa imani alipokea ufunuo wa ile damu. Kaini hakupata ufunuo kama huo (hata ingawa alikuwa na amri) kwa hiyo asingeweza kutoa dhabihu sahihi. Ilikuwa ni ufunuo kutoka kwa Mungu ulioleta tofauti na kumpa Habili uzima wa milele. Sasa unaweza kuchukua yale mchungaji asemayo, ama yale seminari inayofundisha, na ingawa huenda ikafundishwa kwako kwa ufasaha wa maneno, mpaka Mungu atakapokufunulia ya kwamba Yesu ni Kristo, na kwamba ni damu inayokutakasa, na kwamba Mungu ni Mwokozi wako, kamwe hutapata uzima wa milele. Ufunuo wa Kiroho ndio unaofanya jambo hilo.
Sasa nilisema ya kwamba Kitabu hiki cha Ufunuo ni ufunuo wa Yesu na yale anayofanya makanisani kwa zile nyakati saba. Ni ufunuo kwa sababu wanafunzi, wao wenyewe, hawakujua kweli hizi zilizorekodiwa. Haikuwa imefunuliwa hapo awali kwao. Mnakumbuka ya kwamba walimjia Yesu katika Kitabu cha Matendo na kumwuliza, “Je! wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme?” Naye akasema, “Si kazi yako kujua nyakati wala majira.” Watu hao walikuwa wangali wakifikiria juu ya Yesu kuwa na ufalme wa duniani. Lakini ulikuwa ni ufalme wa kiroho ambao alikuwa anaenda kuujenga. Hata Yeye hakuweza kuwaambia kuhusu mahali Pake katika huo, kwa maana Baba hakuwa amemfunulia. Lakini sasa baada ya kifo Chake na kufufuka Kwake, na wakati huu hasa katika huduma Yake ya upatanisho, Yeye anaweza kuweka hapa katika ufunuo huu Wake Mwenyewe kwa Yohana kile utukufu Wake na uwepo wake kanisani ungemaanisha na kufanya.
Katika ufunuo huu anatuambia mwisho wa ibilisi ni nini. Yeye anasimulia jinsi atakavyomshughulikia Ibilisi na kumtupa katika ziwa la moto. Yeye hufunua mwisho wa waovu wanaomfuata Shetani. Na Shetani huchukia jambo hilo.
Je! Umewahi kuona jinsi Shetani anavyochukia vitabu viwili vya Biblia kuliko vingine vyote? Kupitia wanatheolojia wenye mawazo huru na wanasayansi bandia yeye daima anashambulia Kitabu cha Mwanzo na Kitabu cha Ufunuo. Katika vitabu hivi viwili tunaona chimbuko la Shetani, njia zake mbaya sana na maangamizi yake. Hiyo ndiyo sababu anavishambulia. Yeye anachukia kufunuliwa, na katika vitabu hivyo anafunuliwa kwa kile hasa alicho. Yesu alisema kuhusu Shetani, “Yeye hana sehemu ndani Yangu wala sina sehemu ndani yake.” Ibilisi angetaka kuthibitisha jambo hilo tofauti; bali yeye hawezi, kwa hiyo anafanya yote awezayo kuharibu imani katika Neno. Lakini wakati kanisa litakapokataa kumwamini Shetani na liamini ufunuo wa Roho wa Neno, milango ya kuzimu haiwezi kulishinda.
Hebu niweke tu neno ndani hapa kutoka kwenye huduma yangu mwenyewe, kama hamjali. Nyote mnajua ya kwamba karama hii maishani mwangu ni ya kimbinguni. Ni karama ambayo kwayo Roho Mtakatifu anaweza kuyatambua magonjwa, na mawazo ya mioyo ya watu, na mambo mengine yaliyofichwa ambayo ni Mungu pekee angeweza kujua na kisha kunifunulia. Laiti mngeweza kusimama pamoja nami na kuona nyuso za watu wakati Shetani anapojua atafichuliwa. Sasa, si watu ninaozungumzia. Ni kwamba Shetani ameyashikilia katika maisha yao kwa dhambi, kutokujali, na maradhi. Lakini unapaswa kuona nyuso zao. Shetani anajua atafichuliwa, na mabadiliko ya kipekee sana huja juu ya nyuso za watu. Shetani anaogopa. Yeye anajua ya kwamba Roho wa Mungu yu karibu kuwajulisha watu kuhusu matendo yake. Hiyo ndiyo sababu anachukia mikutano hii sana. Wakati majina yanapoitwa na magonjwa yakifunuliwa, Shetani huchukia hilo. Sasa hii ni nini? Si kusoma mawazo, si kuwasiliana mawazo, wala si uchawi. Ni UFUNUO kwa Roho Mtakatifu. Hiyo ndiyo njia pekee ninayoweza kujua jamba hilo. Bila shaka nia ya mtu wa kimwili italiita cho chote kile isipokuwa Roho Mtakatifu.
Hebu niwaonyeshe sababu nyingine kwa nini Shetani huchukia Kitabu hiki cha Ufunuo wa Yesu Kristo kanisani. Yeye anajua ya kwamba Yesu Kristo ni yeye yule jana, na leo, na hata milele, Naye habadiliki. Yeye anajua hilo zaidi sana kuliko asilimia tisini ya wanatheolojia. Yeye anajua ya kwamba kwa kuwa Mungu habadiliki katika tabia Yake, basi Yeye pia habadiliki katika njia Zake. Hivyo basi Shetani anajua kwa hakika ya kwamba lile kanisa la asili pale Pentekoste lenye nguvu za Mungu (Marko kumi na Sita katika matendo) ndilo Kanisa Halisi ambalo Yesu anadai kama Lake. Mambo mengine yote ni ya uongo. Haina budi kuwa hivyo.
Sasa kumbukeni jambo hili. Kristo katika Kanisa la Kweli ni mwendelezo wa KITABU CHA MATENDO. Lakini Kitabu cha Ufunuo kinaonyesha jinsi ambavyo roho wa mpinga-Kristo angeingia kanisani na kulichafua, akilifanya kuwa vuguvugu, la kawaida na lisilo na nguvu. Inamfunua Shetani, ikifunua kazi zake (kujaribu kuangamiza watu wa Mungu na kupuuza neno la Mungu) moja kwa moja hadi wakati atakapotupwa katika ziwa la moto. Yeye anapinga jambo hilo. Hawezi kustahimili jambo hilo. Anajua ya kwamba kama watu wakipata UFUNUO WA KWELI wa KANISA LA KWELI na kile lilicho, msimamo wake ni nini na ya kwamba LINAWEZA KUTENDA ZILE KAZI KUBWA ZAIDI, hilo litakuwa jeshi lisiloweza kushindwa. Kama wakipata ufunuo wa kweli wa hizo roho mbili katika mfumo wa kanisa la Kikristo, na kwa Roho wa Mungu kutambua na kuhimili roho ya mpinga-Kristo, Shetani atakuwa hana nguvu mbele yake. Yeye atashindwa kabisa leo kama wakati Kristo alipopinga kila jitihada zake za kupata nguvu juu Yake jangwani. Naam, Shetani huchukia ufunuo. Lakini sisi tunaupenda huo. Tukiwa na ufunuo wa kweli maishani mwetu, malango ya kuzimu hayawezi kutushinda, bali tutayashinda.
Mtakumbuka ya kwamba nilitaja mwanzoni mwa ujumbe huu kwamba Kitabu hiki tunachojifunza ni ufunuo halisi wa Yesu, Mwenyewe, kanisani na kazi Yake katika nyakati zijazo. Ndipo nikataja ya kwamba inahitaji Roho Mtakatifu kutupa ufunuo la sivyo tutashindwa kuupata. Tukiyaleta pamoja mawazo haya mawili mtaona ya kwamba haitachukua tu kusoma kwa kawaida na kuwaza kukifanya Kitabu hiki kuwa halisi. Itachukua utendaji wa Roho Mtakatifu. Hiyo inamaanisha Kitabu hiki hakiwezi kufunuliwa kwa mtu yeyote ila tabaka maalum la watu. Itahitaji mtu aliye na ono la kinabii. Itahitaji uwezo wa kusikia kutoka kwa Mungu. Itahitaji mafundisho ya kimbinguni, si tu kwa mwanafunzi kulinganisha aya na aya,ingawa jambo hilo ni zuri. Lakini siri inahitaji mafundisho ya Roho ama sivyo halitakuwa dhahiri hata kidogo. Jinsi tunavyohitaji kusikia kutoka kwa Mungu na kujiweka wazi na kujisalimisha kwa Roho kusikia na kujua.
Kama nilivyokwisha sema, Kitabu hiki (Ufunuo) ni ukamilifu wa Maandiko. Hata kimewekwa sawa kabisa katika orodha ya Maandiko; mwishoni. Sasa unaweza kujua kwa nini hasa kinasema ya kwamba mtu ye yote anayekisoma ama hata kukisikia amebarikiwa. Ni ufunuo wa Mungu utakaokupa mamlaka juu ya ibilisi. Nawe unaweza kuona ni kwa nini wale ambao wangeongeza ama kuondoa kutoka kwake wangelaaniwa. Ingebidi kuwa hivyo, kwa maana ni nani anayeweza kuongeza ama kuondoa ufunuo mkamilifu wa Mungu na kumshinda adui? Ni rahisi hivyo. Hakuna kitu kilicho na nguvu za ushindi namna hiyo kama ufunuo wa Neno. Mnaona, katika aya ya tatu baraka inatangazwa kwa wale watakaokitegea sikio maalum Kitabu hiki. Nafikiri jambo hili linazungumzia desturi ya Agano la Kale kuhusu makuhani kuwasomea kusanyiko Neno asubuhi. Mnaona, wengi hawangeweza kusoma kwa hiyo ilibidi kasisi awasomee. Mradi tu lilikuwa ni Neno, baraka ilikuwapo. Haikujalisha kama ilisomwa au kusikilizwa.
“Wakati u karibu.” Wakati haukuwa karibu hapo awali. Katika hekima na utaratibu wa Mungu ufunuo huu mkuu (ingawa ulijulikana kikamilifu na Mungu) usingeweza kuja kabla ya wakati huu. Kwa hiyo tunajifunza kanuni fulani mara moja-ufunuo wa Mungu kwa ajili ya kila wakati unaweza kuja katika wakati huo peke yake, na katika wakati maalum. Angalia historia ya Israeli. Ufunuo wa Mungu kwa Musa ulikuja tu katika wakati maalum wa historia, na hata zaidi hasa ulikuja wakati watu walipomlilia Mungu. Yesu, Mwenyewe, alikuja katika wakati mkamilifu, Yeye akiwa Ufunuo mkamilifu wa Uungu. Na katika wakati huu (Laodikia) ufunuo wa Mungu utakuja katika wakati wake. Hautakawia, wala hautakuwa kabla ya wakati wake. Liwazie hili na ulizingatie vizuri, kwa kuwa tuko katika wakati wa mwisho leo.
Kusoma kamili ya akaunti katika...
Ufunuo wa Yesu Kristo.
Kitabu cha Ufunuo.
Itaendelea kwenye ukurasa unaofuata.
(Ufunuo wa Yesu Kristo.)
Ujumbe kitovu...Chagua lugha yako na kupakua ujumbe huru kutoka Ndugu Branham.